Njia tofauti ya kufanya kazi

Kila toleo la Humanitarian Exchange Magazine huanza kwa swali: je, ni mitazamo ya nani inayoongoza mijadala inayoathiri hatua za kibinadamu? Mara nyingi sana, wale walioathirika zaidi na migogoro hiyo hualikwa kutoa mifano au kuthibitisha mijadala iliyopo, lakini ni nadra sana kupewa nafasi ya kuamua ajenda yenyewe. Toleo hili linalenga kufanya mambo kwa namna tofauti. Badala ya kuchagua mada ndani ya Mfumo wa Utekelezaji wa Masuala ya Kibinadamu (HPN), mtandao huu uliwaalika washirika wake – Muungano wa Kuimarisha Ushirikiano (A4EP), Mtandao wa Haki za Wakimbizi Asia na Pasifiki (APRRN), Mtandao wa Kibinadamu wa Kifeministi (FHN), na Kituo cha Asasi za Kijamii na Demokrasia (CCSD) – kuongoza mchakato huo. Kupitia majadiliano kadhaa, walibainisha mada kuu ya toleo hili kutokana na vipaumbele vya utekelezaji, uongozi wa ndani katika usanifu wa kibinadamu unaobadilika, na kuwaleta pamoja waandishi kutoka katika mitandao yao nchini Bangladeshi, Indonesia, Kenya, Palestina, Syria, Thailand na Uturuki. Jukumu la HPN halikuwa kuweka ajenda, bali kuandaa mazingira ya ajenda hiyo kujitokeza kupitia mazungumzo, ushirikiano na ubadilishanaji kati ya nchi zinazoendelea Kwa kufanya hivyo, toleo hili linaakisi azima endelevu ya HPN ya kukuza maarifa yaliyo jumuishi zaidi, ya ushirikiano na yasiyo ya kikoloni, yanayoimarisha ujifunzaji wa watu binafsi na taasisi katika sekta ya kibinadamu.

Aidha, wahusika wa ndani mara nyingi hutarajiwa kuchangia utaalamu wao, mahusiano yao na uzoefu wao bila malipo. Hata hivyo, kufanya hivyo kunahitaji muda, utaalamu na nyenzo za kitaasisi. Kwa toleo hili, waandishi na mitandao ya washirika walipokea msaada wa kifedha kwa michango yao. Huu ulikuwa utambuzi wa makusudi kwamba utaalamu wa ndani una thamani na kwamba ushirikiano wa usawa unapaswa pia kuzingatia usawa katika kutambua na kutuza michango.

Upatikanaji na ujumuishi pia ilikuwa misingi iliyoongoza kazi hii yote, kwani tulijitahidi kuwaalika waandishi kuandika katika lugha waliyohisi ni rahisi zaidi kwao, huku tukitoa msaada kutoka kwa wahariri wenye utaalamu wa kimuktadha na kiisimu. Hali hii ilisababisha makala kuandikwa kwanza kwa Kiingereza na Kiarabu, kabla ya kutafsiriwa kwa Kiarabu na Kiswahili pale ilipohitajika.

Ndani ya Toleo Hili

Kama ilivyoelezwa awali, mada ya toleo hili ni uongozi wa ndani katika mfumo wa kibinadamu unaobadilika, na imekuja kwa wakati muafaka. Mchakato mpya wa mfumo wa kibinadamu umeanzisha tena wito wa kuwepo kwa mwitikio unaoongozwa na wahusika wa ndani na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa. Hata hivyo, mashirika mengi ya ndani na ya kitaifa bado hupokea sehemu ndogo tu ya ufadhili wa kibinadamu na huendelea kutowakilishwa ipasavyo katika maeneo ya kufanya maamuzi. Makala katika toleo hili yanavuka mipaka ya mijadala ya kawaida na kuchunguza namna uongozi wa ndani unavyoonekana katika utekelezaji halisi. Yanaonyesha jinsi jamii na mashirika ya ndani yanavyokabiliana na mazingira yanayobadilika ya mfumo wa kibinadamu, yakipinga miundo ya mamlaka iliyopo na kufikiria upya namna ushirikiano unavyoweza kujengwa. Kwa pamoja, makala haya yanatoa sio tu taswira ya usanifu unaobadilika wa mfumo wa kibinadamu, bali pia yanatoa maarifa muhimu kuhusu jinsi mustakabali wenye usawa zaidi na wenye ufanisi zaidi wa hatua za kibinadamu unavyoweza kuwa.

Toleo linaanza na makala ya Rajeev Jha kutoka A4EP anayechunguza vikwazo vya kimuundo vinavyoendelea kuzuia uongozi wa ndani hata wakati wa mchakato wa kuanzisha tena mfumo wa kibinadamu. Moriab Gerges Haddo, Narges Ardwan na Muhammad Al-Kajak kutoka CCSD wanaendelea kuchambua pengo lililopo kati ya kauli kuhusu ujanibishaji na utekelezaji wake, wakitumia uzoefu wa miaka mitatu wa kusaidia zaidi ya mashirika 50 ya Syria.

Makala mawili yanayofuata yanaangazia simulizi za jamii zilizohamishwa pamoja na mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, ambayo mara nyingi hupuuzwa katika mijadala inayohusu ujanibishaji. Baqir Bayani kutoka APRRN anachunguza jinsi mifumo iliyopo ya ujanibishaji inavyoendelea kuyaweka pembeni mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, licha ya jukumu lao kama wahudumu wa kwanza na wadau wanaoaminiwa na jamii katika nchi kama vile Indonesia na Thailand. Huku Khair Ullah na Ahtaram Shin kutoka APRRN wanategemea uzoefu wa mashirika yanayoongozwa na wakimbizi huko Cox’s Bazar, Bangladeshi, kuonyesha mchango wao katika mwitikio wa dharura, elimu na ulinzi huku wakibainisha vikwazo vya kimuundo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi.

Licha ya changamoto hizi, makala kadhaa yanaonyesha jinsi wahusika wa ndani wanavyoendelea kuongoza katika hatua za mwitikio. Ohaila Shomar and Majeda Saqqa from FHN wanatafakari kazi ya mashirika yanayoongozwa na wanawake nchini Palestina na jinsi yalivyorekebisha programu na huduma zao ili kukabiliana na kuongezeka kwa vurugu, uhamishaji wa watu na mahitaji ya kibinadamu. Anila Noor na Madina Yunis FHN wanaonesha mbinu ya Kente Threads inayojaribiwa nchini Kenya, ambayo inaonyesha jinsi wanawkutoka ake wa Kenya waliohamishwa wanavyozalisha na kutumia data zao wenyewe ili kufanya maamuzi yanayohusu mabadiliko ya tabianchi na hatua za kibinadamu.

Viongozi wa ndani wa kibinadamu pia wanajitokeza kupitia watu ambao mara nyingi huonekana tu kama wapokeaji wa misaada. Sara Bahsass kutoka CCSD anachunguza mbinu inayoongozwa na jamii nchini Syria inayowezesha jamii kutambua mahitaji yao na kuyashughulikia. Areej Al-Mohammad kutoka CCSD anaangazia wakimbizi wa Syria nchini Uturuki na jinsi walivyobadilika kutoka kuwa wapokeaji wa misaada hadi kuwa wahusika wa hatua za kibinadamu. Makala haya yanapinga mtazamo wa kawaida unaotenganisha watoa misaada na wapokeaji wa misaada, na yanaonyesha kwamba watu walioathiriwa si washiriki tu wa mwitikio wa kibinadamu, bali pia ni viongozi kwa uwezo wao wenyewe.

Toleo hili pia linachunguza juhudi za kubadilisha mahusiano ya ufadhili. Subin Mulmi kutoka APRRN anachambua Mfuko wa Kimataifa wa Kukabiliana na Ukosefu wa Uraia, ambao hutoa ufadhili unaobadilika, wa miaka mingi na usio na masharti kwa makundi yasiyo rasmi ya ngazi ya jamii yanayoshughulikia tatizo la ukosefu wa uraia, ambayo huenda hayajasajiliwa rasmi au hayana uwezo wa kufikia njia za kawaida za ufadhili. Amrita Paul kutoka APRRN anachunguza nafasi ya mtandao huo katika kusaidia mashirika yanayoongozwa na wakimbizi na yale yanayotegemea jamii kupata na kusimamia fedha za pamoja, akionyesha fursa zilizopo pamoja na vikwazo vinavyoendelea kuwepo ndani ya mifumo ya ufadhili wa kibinadamu.

Mafunzo muhimu

Ingawa makala haya yanatokana na simulizi kutoka mazingira mbalimbali—kuanzia Syria na Palestina hadi Kenya, Bangladesh na eneo la Asia-Pasifiki—yanaafikiana kuhusu ujumbe mmoja wa msingi: uongozi wa ndani tayari upo. Jamii, mashirika yanayoongozwa na wakimbizi, mipango inayoongozwa na wanawake na asasi za kiraia za ndani hazisubiri kutambuliwa kimataifa; tayari zinaongoza hatua za mwitikio, zinabuni suluhisho, zinajirekebisha na kuzisaidia jamii zao kustahimili migogoro. Kinachoendelea kuwazuia si ukosefu wa uwezo, bali ni usanifu wa mfumo wa kibinadamu ambao mara nyingi hujikita katika kuelekeza ufadhili, kufanya maamuzi na kutoa uhalali katika taasisi za kimataifa.

Katika makala yote, waandishi wanabainisha vikwazo vinavyojirudia, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ufadhili isiyobadilika, kutengwa katika maeneo ya uratibu na utawala, masharti mazito ya uzingatiaji wa taratibu, pamoja na vizuizi vya kisheria na kisiasa vinavyozuia wahusika wengi wa ndani kupata rasilimali moja kwa moja. Wakati huo huo, makala haya yanatoa mifano yenye ushawishi ya mbinu mbadala, yakionyesha jinsi ufadhili unaobadilika, ushirikiano unaotegemea uaminifu, ufanyaji wa maamuzi kwa ushirikiano, mwitikio unaoongozwa na jamii na utambuzi wa thamani ya uzoefu wa maisha unavyozalisha hatua za kibinadamu zenye ufanisi zaidi, uwajibikaji mkubwa na uendelevu. Kwa pamoja, michango hii inaipa sekta ya kibinadamu changamoto ya kufanya zaidi ya lugha ya ujanibishaji pekee na kuelekea katika ugawaji wa kweli wa mamlaka, rasilimali na maarifa, ambapo uongozi wa ndani unatambuliwa sio kama matarajio ya baadaye, bali kama uhalisia uliopo tayari unaostahili kuunda mustakabali wa hatua za kibinadamu.

Shukrani

Toleo hili limekuwa zao la ushirikiano wa kweli. Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa mashirika washirika wetu na waandishi wote ambao kwa ukarimu walishiriki maarifa yao, uzoefu wao na tafakuri zao. Tunawashukuru kwa namna ya pekee timu yetu ya uhariri pamoja na watafsiri, Tamarind Language Services Ltd na Hashem el Hashem, ambao utaalamu wao wa kimuktadha na kiisimu ulihakikisha kwamba mawazo yaliyowasilishwa hapa yaliwafikia wasomaji wa Kiarabu, Kiswahili na Kiingereza huku yakihifadhi uhalisia na sauti ya kila mchango.

Catherine Komuhangi
Meneja wa Uratibu wa HPN

Serena Abi Khalil
Mkuu wa Maendeleo na Ushirikiano wa HPN

Can you help translate this article?

We want to reach as many people as possible. If you can help translate this article, get in touch.
Contact us

Did you find everything you were looking for?

Your valuable input helps us shape the future of HPN.

Would you like to write for us?

HPN accepts submissions from its members. If you would like to write for us, follow Our Guidance below.
Our Guidance