Kati ya ukame na mafuriko: udhaifu wa ‘ustahimilivu’ katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma

June 25, 2025

Dieu Merci Luundo

Sunday Amum

Paul O'Keeffe

Wakimbizi wakifanya kazi shambani.

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma, iliyoanzishwa mwaka wa 1992 katika eneo la kaskazini-magharibi mwa Kenya, ni makazi ya wakimbizi zaidi ya 302,000, wengi wao wakitoka Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mwanzoni, kambi hii iliundwa kama makazi ya muda kwa wavulana wa Kisudani waliokuwa wakikimbia Vita vya Pili vya Kiraia vya Sudan mapema miaka ya 1990, Kakuma sasa imekuwa makazi ya kudumu yenye miundombinu finyu na inafanana na mjiimkubwa wa mabanda ulioenea, wenye matatizo mengi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Tukizingatia mzozo unaoendelea wa kimataifa wa janga la ufadhili wa misaada ya kibinadamu na maendeleo, kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi, mabadiliko ya tabianchi na vurugu za mara kwa mara za kisiasa katika eneo hili, wakaazi wa Kakuma wanakabiliwa na shinikizo kubwa zaidi la kujitegemea huku mgao wa chakula ukizidi kupungua na wajibu wa ulinzi kutoka kwa jamii ya kimataifa ukizidi kudhoofika. Zaidi ya hayo, matukio ya hivi karibuni – hasa mafuriko ya hivi majuzi yaliyofuata kipindi cha baada ya ukame wa miaka mitano – yanaonyesha kuwa wakimbizi wanakabiliwa na vikwazo vikubwa katika kufanya hivyo.

Kwa kuwa mgao wa chakula umepunguzwa hadi chini ya 45% ya mahitaji ya chini ya kalori kwa siku, wakimbizi wengi wamehangaika kutafuta njia za kuendelea kuishi.

Ziwa lililo karibu lilitoa ardhi yenye rutuba kwa kiasi pamoja na kutoa upatikanaji rahisi wa maji kupitia kuchimba visima vya chini ya ardhi, kwa ajili ya wakulima ili wapande mimea, ingawa kwa hatari kubwa. Mvua za ghafla ziliponyesha, mimea hii na mashamba haya ya kimsingi yaliangamizwa, na hivyo kuharibu maisha ya mamia ya watu. Katika makala hii, tunatumai kuangazia tatizo hili kwa kueleza jinsi udhaifu wa kimfumo na kutelekezwa kwa juhudi za kimataifa kunavyozidisha migogoro ya aina hii, na kupendekeza mabadiliko ya mitazamo ya juhudi za kibinadamu kuelekea kuunga mkono juhudi za ndani na mashinani zinazozingatia hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabiancchi, ambazo zina nafasi nzuri zaidi ya kuwa na ufanisi katika muda mrefu.

Maisha ya kujitegemea na ya kilimo yamo hatarini

Huku wakimbizi wakikabiliwa na mgao wa chakula unaopungua na fursa chache za ajira, kilimo cha mazao karibu na ziwa la msimu lilikuwa jaribio la mwisho kwa wengi kujaribu kuendeleza maisha yao wakiwa uhamishoni. Hii ilikuwa ni mbinu ya kujitegemea iliyochochewa kwa njia nyingi na kauli ya kusifika ya ‘ustahimilivu wa wakimbizi’ tunayosoma sana kuihusu katika nyaraka za sera na mijadala ya maendeleo ya kibinadamu duniani kote.

Udongo wa ziwa na viwango vya maji vya chini ardhini viliifanya eneo hilo kufaa kwa kilimo cha muda mfupi na, jambo muhimu zaidi, kuchimba visima ili kupata maji yanayohitajika sana wakati wa ukame unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi. Wakimbizi walipanda moringa, murere, okra, sukuma wiki, mchicha, amaranth, kunde, viazi vitamu, mihogo, mahindi, nyanya na vitunguu – vyote muhimu kwa lishe ya familia na mauzo katika masoko yasiyo rasmi.

Lakini, kama wakimbizi wanavyojua sasa, mashamba haya yalijengwa kwenye ardhi hatari. Mvua kubwa ya hivi karibuni – iliyomaliza ukame wa muda mrefu uliovunja rekodi – ilisababisha mafuriko katika eneo hilo, ikaharibu mazao, pamoja na vyanzo vya riziki na matumaini kwa usiku mmoja. Kulingana na mahojiano tuliyofanya na wakimbizi mwezi Aprili 2025, familia nyingi zilipoteza kila kitu: mimea yao, mbegu, vifaa vya kilimo, na miezi ya kazi yao Ukosefu wa mwitikio wa dharura au hata dalili za kuzingatiwa kutoka kwa mashirika ya misaada ya kibinadamu ya kimataifa yanayofanya kazi kambini Kakuma unazidi kuwasukuma wakazi ambao tayari ni wanyonge wanaoishi katika umasikini wa hali ya juu.

Mabadiliko ya tabianchi na udhaifu

Kakuma iko katika Kaunti ya Turkana, mojawapo ya maeneo yenye ukame zaidi nchini kenya. Eneo hilo limekumbwa na misimu mitano mfululizo ya mvua kufeli kunyesha (2019–2023), hali ambayo imesababisha mimea kufa, mifugo kufa, uhaba wa maji, na shinikizo kubwa kwa kambi hii ya wakimbizi kutoa makazi kwa idadi inayoongezeka ya watu waliokumbwa na majanga kama hayo. Mtindo huu unaenda sambamba na hali pana ya Pembe ya Afrika inayohusishwa na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua isiyotabirika, joto kali kupita kiasi na mafuriko ya ghafla.

Mvua kali ya 2024/25 ilinyesha kwa vurugu kali. Mvua ambayo kwa kawaida hupokelewa kwa furaha ilisababisha mafuriko katika eneo hilo ambalo halikuwa tayari, na iliwapata wakazi wa eneo hilo bila tahadhari, ikisomba mimea, kuzamisha vyoo na kuharibu mipango ya jamii ambayo wakimbizi walikuwa wameanza kutegemea. Kwa maoni yetu, ukosefu wa upangaji wa kimazingira au mifumo ya onyo kambini Kakuma, pamoja na mwitiko wa kuchukua hatua baada ya janga badala ya mwitikio wa kujiandaa mapema, kwa ujumla unaonyesha kushindwa kwa serikali kujumuisha hatua za kukabiliana na matatizo ya tabianchi katika mifumo ya ulinzi wa wakimbizi.

Sauti za wakimbizi wanaoishi bonde la mafuriko

Kwa wakulima wengi wakimbizi, mafuriko hayakuwa tu janga la kimazingira, bali pia hasara kwa watu binafsi na ya kudumu. ‘Ni kama kufa tena na tena,’ Nyange Mauridi Wilongela alisema, mkulima wa Kongo aliyepanda amaranthi, majani ya muhogo, na boga kwenye bonde lenye rutuba la ziwa. ‘Tulitegemea ardhi hiyo. Ilitusaidia kununua sabuni, makaa, na kadi za simu – vitu ambavyo mgao wa chakula hautupatii.’ Shamba lake, lililoko takriban mita 30 kutoka kwenye mto wa msimu (Mto Laga), lilichaguliwa kwa sababu ya udongo wake wenye rutuba na ukaribu na maji ya chini ya ardhi. ‘Kisha Mto Laga ulifurika na kuondoa kila kitu.’

Wengine kama Peter Deng Hul, mkimbizi kutoka Sudan Kusini aliyekuwa amewekeza mapato ya duka lake dogo katika kilimo, walipoteza sana pia. ‘Mimi nilikuwa muuzaji mkubwa wa majani ya moringa katika eneo langu. Kilimo kilikuwa njia yangu ya kulea familia yangu. Kisha mvua ikaja, na mimea yangu yote ikatoweka kwa usiku mmoja.’ Deng, ambaye hata alikuwa amechimba mifereji midogo ya umwagiliaji na unyunyuziaji maji ili kupeleka maji ya jamii kwenye shamba lake, lakini hakuna kitu chochote ambacho kingeweza kumwandaa kwa mto kufurika na kuvuja pamoja na kuharibu kazi ya miezi kadhaa.

Adau Bol Beliu, pia kutoka Sudan Kusini, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kupoteza makazi yao pamoja na shamba lake. ‘Nimekuwa nikilima kwa miaka 11. Msimu huu, mvua ilikuwa mbaya kuliko yoyote niliyowahi kuona,’ alisema. ‘Shamba letu lilinisaidia kuwalisha watoto wangu. Mgao wa chakula haukamilishi hata nusu ya mwezi.’

Wakulima waliohojiwa walisisitiza mara kwa mara ukosefu wa njia mbadala zinazowezekana za kujikimu. Mashamba madogo kwenye makazi hayawezi kuwawezesha kutimiza majukumu kutokana na ukosefu wa nafasi, wanyama, na hatari ya kemikali kwa watoto. ‘Hata nikijaribu kupanda mimea nyumbani, kuku huharibu kila kitu,’ Beliu alisema. Wanatoa wito wa kupewa ardhi salama, mafunzo, vifaa, na ulinzi dhidi ya majanga mengine ya mabadiliko ya tabianchi.

Maelezo haya ya maisha ya watu binafsi yanaangazia kwa nguvu hali halisi ya maisha ya wakimbizi huku matamshi ya sera kuhusu ‘ustahimilivu’ yakipewa umuhimu. Bila msaada wa kuwawezesha wakulima kufanya a kilimo kinachokabiliana na na mabadiliko ya tabianchi na kinachoongozwa na wakimbizi wenyewe, wakazi wa Kakuma wanabaki bila chakula wala matumaini ya baadaye.

Tunachopendekeza

Mitazamo ya maendeleo inayoongozwa na wakimbizi

Mashirika ya maendeleo ya ndani na mashinani yanayoongozwa na wakimbizi yanatoa mbinu zenye maarifa, ambazo ni muhimu na zenye uhalisia ambazo taasisi zinazoendesha maendeleo kutoka juu haziwezi kuiga. Zaidi ya yote, kupitia ushirikishwaji halisi wa jamii na uongozi wa moja kwa moja, mashirika haya yanatoa matumaini na mwongozo wa jinsi ‘ustahimilivu’ unafaa kuwa. Mfano mmoja ni mradi wetu, Vijana Twaweza Community (VTC) shirika moja la mashinani linalowaleta pamoja wakimbizi walioko kambini Kakuma, shirika hili linasaidiwa na mashirika wenza ya kimataifa, yanayokuza kilimo, ufugaji wa kuku, samaki na sungura ndani na nje ya Kakuma. Mradi wetu mkuu wa Fishing in the Desert, unalenga ufugaji wa samaki kwa lengo la kutoa protini inayohitajika sana kwa watu wa Kakuma. Mnamo mwaka 2024, VTC ililisha zaidi ya familia 500 na ikazindua mradi wa Inua Mama kwa ajili ya kuwafundisha wanawake viongozi wa familia kuwa wafugaji wa kuku. Kwa msaada wa Crédit Agricole Assurances na Chuo Kikuu cha Jiji la Dublin, programu hiyo iliwafundisha wanawake 10 katika mwaka wake wa kwanza na sasa imepanuka hadi kuwafundisha wanawake 30 mwaka wa 2025.

Washiriki hupokea vifaranga, chakula cha kuku, mafunzo na vifaa vya kuanzisha mradi. Mfumo huu unakuza lishe, uwezeshaji wa kiuchumi, mbinu endelevu za kilimo na uongozi wa jamii katika eneo. VTC pia inajihusisha na ufugaji wa sungura, ulishaji wa panzi na shamba za mboga, kwa kutoa msisitizo kwa mifumo midogo inayoweza kuigwa kwa urahisi, inayotumia maji kidogo, miundombinu rahisi, na iliyobuniwa kulingana na mazingira ya eneo husika. Jitihada hizi, ingawa ni ndogo kwa kiwango, zinatoa njia endelevu ya kujipatia riziki na kusaidia kupunguza uchovu wa misaada ya kutoka juu kwenda chini.

Elimu zaidi na bora kwa ajili ya maendeleo endelevu

Elimu kwa ajili ya maendeleo endelevu (ESD) bado haipewi msaada wa kutosha katika mazingira ya wakimbizi na migogoro kama vile mazingira ya Kakuma, ambako mahitaji ya kuishi siku baada ya siku hupewa kipaumbele kuliko mipango ya muda mrefu. Hata hivyo, tukizngatia majanga ya asili na yale yanayosababishwa na binadamu, uhaba wa chakula, na kusambaratika kwa miundombinu ya misaada ya kibinadamu, elimu mara nyingi huwa suluhisho pekee linalopatikana na ambalo kila mtu anakubali kuwa huleta mabadiliko chanya.

Kuimarisha na kupanua nafasi ya elimu kwa maendeleo endelevu (ESD)kunahitaji kwenda zaidi ya shule za kawaida na kujumuisha mafunzo ya kiufundi, sayansi ya kilimo, na ujuzi wa ujasiriamali unaoendana na muktadha wa eneo husika. Mikakati ya elimu inayoongozwa na jamii, kama Mpango wa Mafunzo ya Ufugaji wa Kuku wa Inua Mama wa VTC, zimeonyesha matumaini makubwa katika eneo hili – kwa kutoa chaguo mbadala wa vitendo, vinavyohusiana moja kwa moja na mazingira husika, na vya gharama nafuu ikilinganishwa na mipango ya maendeleo inayoendeshwa kutoka juu na taasisi.

Hata hivyo, vikwazo vya kimfumo bado vinaendelea kuwepo: mipango ya elimu inayotegemea jamii haipati ufadhili wa kutosha, na mbinu za mashinani mara nyingi huwekwa pembeni na mifumo ya misaada ya kibinadamu inayotoa kipaumbele kwa matarajio makubwa badala ya uhalisia. Kuna uhitaji wa dharura wa mikakati ya elimu iliyo inayofaa jamii kienyeji zaidi na inayowezekana ambayo inawawezesha wakimbizi ( kifedha na kitakwimu) kuwa mawakala wa mabadiliko – hasa wakati ambapo mifumo ya misaada ya kimataifa inaendelea kupungua.

Mapungufu ya Kimuundo katika miundombinu ya misaada ya kibinadamu na maendeleo ya kimataifa

Awamu ya hivi karibuni ya kupunguzwa kwa mgao wa chakula na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inamaanisha kuwa wakazi wa Kakuma sasa wanapokea chini ya kilokalori 945 kwa siku. Idadi hii iko chini sana ya Kiwango cha Sphere cha kalori 2,100 kcal/kwa siku kwa ajili ya mahitaji ya nishati ya mtu mzima katika miktadha ya kibinadamu. Ukosefu wa chakula umesababisha utapiamlo na lishe duni, maandamano, ghasia kati ya jamii, wanafunzi kuacha shule, na matatizo mengine mbalimbali ya kijamii. Wakati huo huo, simulizi kuu kutoka kwa mashirika ya misaada na maendeleo zinabaki kuwa matarajio kwamba wakimbizi wajitegemee, bila rasilimali za kutosha kama ardhi, vifaa, au mafunzo.

Mabadiliko ya wafadhili kutoka kwa maendeleo ya muda mrefu katika mazingira ya migogoro – hasa wakati ufadhili kutoka Ulaya na Amerika Kaskazini unaelekezwa kwa vipaumbele vya ndani – yamewaacha wakimbizi katika hali mbaya kuliko wakati wowote uliopita. Aidha, msaada na mipango ya maendeleo mara nyingi hukosolewa kwa kuwa imegawanyika sana, ikifuata mwelekeo wa kisiasa wa hivi karibuni na mara chache kuzingatia muktadha maalum. Zaidi ya hayo, vikwazo kutoka nchi mwenyeji, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa isiyo thabiti, ushindani mkubwa kwa rasilimali adimu, mipaka katika umiliki wa ardhi na vibali vya kazi, vinazidi kudhoofisha uwezo wa wakimbizi kujitegemea.

Mwishowe, ili maendeleo endelevu yawe tiba kamili, maisha ya kujikimu lazima yashirikishwe upya katika kambi za wakimbizi kama haki, si kama usaidizi. Hii itamaanisha kuingiza mageuzi ya kisheria, upatikanaji wa masoko, fursa za elimu na msaada wa kisaikolojia katika mikakati ya baadaye ya misaada ya kibinadamu na maendeleo katika miundombinu ya kimataifa ya misaada na maendeleo.

Mapendekezo ya sera na utekelezaji

  1. Kurejesha viwango kamili vya mgao wa chakula: Maombi ya dharura yanahitajika ili kurejesha mgao wa chakula kufikia viwango vya chini vya kibinadamu vinavyokubalika. Wafadhili wa kimataifa wanapaswa kutenga ufadhili mahsusi kwa ajili ya migogoro ya wakimbizi ya muda mrefu.
  2. Kusaidia mashirika yanayoongozwa na wakimbizi: Ongeza ufadhili na msaada wa kiufundi kwa makundi kama VTC ili kuendeleza maendeleo ya kweli na ya kudumu kutoka mashinani. Wafadhili wanapaswa kurahisisha upatikanaji wa ruzuku kwa miradi inayoendeshwa na wakimbizi.
  3. Kuwekeza katika kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi: Jenga vitalu vya kupanda vilivyoinuliwa, wekeza kwenye mifumo ya kuzuia mafuriko, anzisha mbegu zinazostahimili ukame na mafuriko, na panua matumizi ya umwagiliaji wa matone. Jaribu mifumo ya onyo la mapema na elimu ya kilimo inayobadilika kulingana na hali ya mazingira.
  4. Kujumuisha mafunzo ya ufundi katika elimu: Panua upatikanaji wa elimu katika mazingira ya wakimbizi na toa kipaumbele kwa elimu ya kiufundi katika kilimo na maendeleo ya biashara. Unganisha programu za elimu na huduma za mikopo midogo na rasilimali kama vile programu ya Mafunzo yaUfugaji wa Kuku ya Inua Mama ya VTC.
  5. Kuboresha ushirikiano na uratibu: Mashirika ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa yasiyo ya kiserikali (INGOs), na serikali lazima waandae kwa pamoja mikakati na wakimbizi kwa ushirikiano na mashirika yanayoongozwa na jamii.

    Hitimisho

    Tatizo la ukame na mafuriko huko Kakuma si tukio la mabadiliko ya tabianchi pekee – ni matokeo ya kushindwa kwa mifumo mingi kwa wakati mmoja, ikiwemo mzigo mkubwa wa kupita uwezo wa mfumo uliopo na ukosefu wa mipango ya muda mrefu. Wakimbizi waliokabiliana kwa juhudi na kupunguzwa kwa mgao wa chakula kwa kulima maeneo ya mabonde ya maziwa – bila makosa yao wenyewe – waliona kazi yao ikiharibiwa kabisa na mafuriko yaliyosababishwa na mabadiliko ya tabianchi kwa muda mfupi mno. Kutengwa kwao kutoka mifumo ya kitaifa, miundombinu ya msaada isiyofadhiliwa vya kutosha, na ukosefu wa zana za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kumezidisha janga hili.

    Hata hivyo, jamii za wakimbizi si wahanga wasio na msaada. Kupitia miradi kama ya VTC na mingine mingi ya maendeleo inayoongozwa na jamii, mfano tofauti sasa unaonekana – mfano unaojengwa kutokana na uwezo wa jamii kushirikiana kwa pamoja, jamii kujijenga kwa kuboresha hali zilizopo, ushirikishwaji wa jamiii nzima na ustahimilivu wa kweli. Kwa watendaji wa misaada ya kibinadamu, wajibu uko wazi: sikilizeni, wekezeni katika ngazi ya jamii, na mvuke mbali na mfumo wa kuamrisha kutoka juu kwenda hadi kwenye ushirikiano wa kweli.


    Dieu Merci Luundo ni mwenyekiti wa jamii ya Vijana Twaweza Community kambini Kakuma.

    Sunday Amum ni mshiriki wa Jamii Vijana Twaweza huko Kakuma.

    Paul O’Keeffe ni msomi, mwandishi na mtaalamu wa maendeleo endelevu kutoka Ireland.

    Comments

    Thanks for choosing to leave a comment. Please keep in mind that all comments are moderated according to our comment policy.

    Let's have a personal and meaningful conversation.

    Can you help translate this article?

    We want to reach as many people as possible. If you can help translate this article, get in touch.
    Contact us

    Did you find everything you were looking for?

    Your valuable input helps us shape the future of HPN.

    Would you like to write for us?

    HPN accepts submissions from its members. If you would like to write for us, follow Our Guidance below.
    Our Guidance